Kiungo tegemezi wa Simba SC aingizwa mjini na wahuni wa Kariakoo

Kiungo wa klabu ya Simba, Mghana James Kotei amekaribishwa nchini Tanzania kwa kulizwa na wezi wa mitaa ya Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es salaam kwa kuibiwa simu yake ya mkononi.

James Kotei
Kiungo huyo akiwa maeneo ya mitaa ya Msimbazi alijikuta akiingia mikononi mwa vibaka waliobobea kwa wizi na kumuibia simu ya mkononi yenye thamani ya Sh milioni 1.4, ambayo alipewa zawadi na mmoja wa wanachama wa Simba siku chache kabla ya mechi ya Ngao ya Jamii iliyoikutanisha Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Maelezo kutoka kwa mtu wa karibu wa klabu hiyo amedai kuwa mchezaji huyo alistuka baada ya kufika makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Msimbazi akitokea Hotelini alikofikia na kujikuta hana simu.
“Baada ya kutembea hatua chache hivi alipita sehemu kununua juisi ya miwa na hapo ndipo akajikuta akiibiwa simu hiyo, Simu hiyo alikuwa ameweka katika mfuko wa nyuma wa begi lake la mgongoni alilokuwa amebebea vifaa vyake vya mazoezi,” amesema mtu wa karibu wa klabu hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Alipoulizwa Kotei kuhusiana na suala hilo amekiri wazi kuwa ni kweli amepatwa na balaa hilo na kudai kuwa amepoteza mawasiliano yake muhimu.

“Ni kweli kabisa nimeibiwa simu jana (juzi-Jumatatu), nilipokuwa nikitokea mazoezini, imeniuma sana kwani nimepoteza mawasiliano yangu mengi,“amesema Kotei kwenye mahojiano yake na gazeti la Championi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.