Makala: Mambo Matano kuhusu ngoma ya Alikiba ‘Seduce Me’

Baada ya ukimya wa mwaka mmoja na zaidi, hatimaye August 25, 2017 msanii Alikiba alitoa ngoma yake mpya ‘Seduce Me’. Ngoma hii imekuja kujibu vilio vya mashabiki wake ambao kila siku walikuwa wakimuomba kufanya hivyo.

Mashabiki wa Alikiba walikuwa wakipata kigugumizi kumteta hasa pale walipokuwa wakizodolewa na washindani wa msanii huyo ambao kila mara wamekuwa wakitoa ngoma. Hivyo basi Seduce Me imekuja kuivua aibu yao na kuwapa ujasiri wa kutembea kifua mbele kumtetea msanii wao na kuonyesha maana kamili ya team Kiba.
Nikiwa kama mfuatiliaji na mpenzi wa muziki wa Bongo Flava nadhubutu kusema wimbo ni mkali tena katika kiwango cha juu kabisa kuwahi kutokea. Ni wimbo tulivyo ambao unahitaji muda tulivu, akili na moyo tulivu ili kuweza kufaidi melody nzuri na ujumbe wake.
Kutokana na uzito wa msanii huyu na kile kilichokuwa kikisubiriwa kwa muda mrefu, tunakuletea vitu vitano ambavyo vina uhusiano wa karibu na ngoma hiyo (Seduce Me).
  1. Ngoma ya kwanza akiwa Boss RockStar4000
Awali Alikiba alikuwa msanii wa kawaida chini ya RockStar4000 pamoja na Lady Jadee na Barakah The Prince ambaye alikuja kujitoa hivi karibuni.
July 4 mwaka huu Rockstar4000 walimtangaza Alikiba kuwa ni miongoni mwa wamiliki wa kampuni ya Rockstar4000 Music Entertainment Co & Rockstar Television. Msanii huyu ambaye amekuwa chini ya RockStar400 kwa miaka sita pia atakuwa Director of Music and Talents.
Baada ya Alikiba kupata nafasi ya kuwa boss hakusita kumsaini Ommy Dimpoz ambaye wamekuwa wakishirikiana katika kazi. Wawili hawa wameshatoa ngoma kama Nai Nai na Kajiandae, zote za Dimpoz. Weka nukta hapo.
Hivyo basi ngoma mpya ya Alikiba alikuwa ukisubiriwa ili kuangalia improvement yake katika muziki kwa kuzingatia kigezo cha kutoka kuwa msanii wa kawaida hadi kuwa boss.
Wengi waliamini ujio wa ngoma mpya utakuwa wa aina yake kwani boss ana uwezo wa kupendekeza/kuchagua nataka ku-shoot video sehemu fulani na director huyo, nataka kolabo na msanii fulani n.k, ukizingatia RockStar4000 ni kampuni kubwa ya muziki barani Afrika.
Hatimaye paap!!, ngoma hii hapa, kwa ilivyokawaida ya misingi ya dunia hii kila kitu/jambo lazima kuna pande mbili, yaani hasi na chanya, nuru na mwanga n.k. Hivyo ngoma hii wapo waliosema ndiyo na wengine kwa sababu zao wakasema hapana.
Vyovyote itakavyokuwa hii ndio ngoma ya kwanza kwa Alikiba akiwa kama mmoja wa wamiliki wa RockStar4000.
  1. Ngoma ya kwanza baada ya kushinda MTV EMA
Alikiba ndiye msanii wa mwisho kutoka Bongo kushinda tuzo ya MTV EMA ambayo ina heshima yake barani Afrika. Sidhani kama umenialewa, yaani kama tuzo ni ubingwa katika soka au michezo mingine, basi Alikiba ndiye bingwa ‘mtetezi’ kwenye tuzo hizi kwa upande wa Bongo Flava.
Alikiba alikabidhiwa tuzo yake February 17 mwaka huu ingawa rasmi zilitolewa mwaka jana na hili lilisababishwa baada ya Wizkid kutangazwa mshindi ilhali kwenye website ya tuzo hizo, kura zilionesha kuwa ni Alikiba ndiye aliyeshinda.
Lakini baada ya MTV EMA kujua makosa yao, waliamua kumpokonya tuzo ya Best African Act Wizkid na kumpa Alikiba ambaye alistahili kushinda, tuachane na hilo.
Sasa basi Alikiba ametoa ngoma mpya tangu alipopata ushindi huo ukiachana na Aje Remix aliyoitoa masaa kadha mbele baada ya kupokea tuzo hiyo, je itamuwezesha kushinda tena tuzo hiyo au kuteuliwa kushiriki?.
  1. Je Come Back hii ni Man Water tena?
Mwaka 2014 Alikiba alirejea kwa kishindo kikubwa katika Bongo Flava baada ya ukimya wa miaka miwili. Ujio wake uliwa wa ngoma mbili ambazo ni Mwana na Kimasomaso lakini Mwana ndio iliyokuwa kubwa zaidi na yeye ndiye aliipa kipaumbele.
Ngoma ya Mwana ilitengezwa na Producer Man Water ndani ya Combination Sound, kabla ya hapo Man Water alikuwa ameshamtengenezea Alikiba hit ya Dushelele, hivyo Mwana ikawa ya pili. Kwa lugha rahisi tunaweza kusema ujio ule wa Alikiba ambao una historia yake, mchango wa Man Water ni mkubwa na unatambulika na kila mtu.
Hii ni 2017 Alikiba anafanya kitu kama kile tena ila haijaeleweka iwapo Man Water anahusika kwa namna moja au nyingine kwa kuwa kwenye cover ya ngoma na video yake hajaonyesha hilo ila naweza kujenga hoja katika mambo mawili.
Mosi; ukisiliza ngoma (Seduce Me) ya mwanzoni kuna sign tone ya Man Water ambayo amekuwa akiitumia katika ngoma ambazo anatengeneza. Ngoma yoyote ya Bongo unaposikia mwanzoni sauti ya maji kumwagika/kutiririka basi ujue huyo ni Man Water, je ndiye yeye tunayemsikia?.
Pili; Kati ya mwezi mmoja hadi miwili iliyopitia Alikiba aliposti clip ya video Instagram akiwa na producer huyo na kueleza kuna kitu yaani kazi mpya inakuja ingawa baadaye post hiyo ilikuja kufutwa. Pia August 16 Man Water aliposti Instagram cover mbili zenye ujumbe Heart Breaker na Kipusa kitu ambacho Alikiba alifanya pia.
Kwa kuambatanisha hoja zangu mbili hapo juu nitamatishe kwa kusema ujio huu wa pili wa Alikiba kuna ushirika wa Man Water, haijalishi kwa kiwango gani.
  1. Jina la wimbo, ‘changa la macho’
Moja ya vitu vilivyowachanganya wengi ni kutaka kujua jina la ngoma mpya ya Alikiba. Wengi waliamini ngoma mpya ingeitwa Kipusa pindi alipoweka cover yenye jina hilo katika ukurasa wake wa Instagram.
Achilia mbali Kipusa, aliweza kuweka cover zenye maneno kama Heart Breaker na Pasua Kichwa kitu ambacho kilifanya baadhi kuamini tena anaweza kutoa ngoma tatu kwa wakati mmoja, kumbe changa la macho.
Wiki mbili zilizopita katika kipindi cha Shilawadu kinachoruka Clouds TV, watangazaji wa kipindi hicho walifunga safari hadi nyumbani kwa Alikiba. Lengo la safari yao ni kumsaka huyo Kipusa, kujua mengi kuhusu Kipusa.
Walitumia muda mwingi nje wakimngoja Alikiba atoke awaeleze anaposema Kipusa ana maanisha nini na kama ni wimbo unatoka lini. Katika mazungumzo yao ndani ya dakika moja neno Kipusa lilijitokeza zaidi ya mara tatu. Hivyo na wao waliamini ngoma mpya ya Alikiba inaitwa Kipusa, kumbe sivyo.
Mara paap!!ngoma mpya (Seduce Me) hii hapa, Kipusa Heart Breaker na Kichwa ni maneno tu ya kawaida ambayo yapo katika ngoma hiyo ingawa yamejirudia mara kwa mara.
  1. Ushindani mkubwa
Ngoma Seduce Me imekutana na ushindani mkubwa sana ukilinganisha na ujio wa Mwana mwaka 2014. Ngoma hii imekuja kipindi ambacho ushindani kati ya Alikiba na Diamond upo juu zaidi.
Imetoka wakati team zinazoshabikia wasanii hawa zimekuwa na nguvu kubwa kuliko katika mitandao ya kijamii, ni team ambazo zina ukichaa wa aina yake katika muziki, ukichaa uliojenga ‘kilema’ kwamba hapa ninaposhabikia ndio bora zaidi na hakuna mwingine kamwe au upande wa pili kushinda hapa nilipo.
Alikiba na Diamond wanatajwa kama wasanii wenye ushindani mkubwa zaidi kwa sasa katika Bongo Flava, wamejijengea fan base yao kila kona ila kwenye mitandao ni hatari tupu, wameweza kuchizisha mashabiki wao kupitia muziki kadiri wawezavyo. Twende pole pole.
August 25 mwaka huu ndipo Alikiba alitoa wimbo ‘Seduce Me’ na uliweza kufikisha views zaidi 500, 000 katika mtandao wa YouTube ndani ya saa 24 na kushika namba katika trending. Wakati Alikiba akichekelea hafikia hatua hiyo, siku iliyofuata Diamond akishirikiana na Harmonize, Rich Mavoko, Rayvanny, Queen Darleen na Maromboso wakatoa ngoma ‘Zilipendwa’.

Hii ni jana saa 12 jioni katika mtandao wa Youtube
Hivyo basi, ngoma ‘Seduce Me’ ikapata ushindani kamili kutoka kwa mshindani kamili na aliyetarajiwa. Ingawa maneno ni mengi kuhusu ngoma hizi mbili kufuatana ila hii ndio maana ya ushindani wenye tija kwa wasanii na mashabiki wao na si vinginevyo.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.