Huddah, Wema Wanunua Ugomvi wa Mobetto na Zari Waamua Kuingilia Kati
Wakati kitendawili cha nani ni baba wa mtoto wa pili wa mwanamitindo Hamisa Mobeto kikiteguliwa baada ya mwenyewe kukiri hadharani jana, wasichana wawili ambao waliwahi kutoka kimapenzi na baba wa mtoto huyo, Wema Sepetu na Huddah Monroe wamejitokeza na kuingilia ugomvi kati ya Zarinah Hassan ‘Zari’ na Hamisa Mobeto.
Kwa muda mrefu kumekuwa na tetesi kuwa mtoto huyo wa Hamisa aliyepewa jina la Abdulatif Nasibu Abdul ni wa msanii mmoja mkubwa wa muziki wa kizazi kipya, ingawa kwa muda alikuwa akikanusha. Lakini jana, akihojiwa na kituo kimoja cha redio jijini, msanii huyo ambaye pia amezaa watoto wawili na Zari, alikiri kushiriki mapenzi na mwanamitindo huyo na kwamba amekuwa pia akimhudumia kwa kumpa kiasi cha shilingi laki tano kwa wiki, sambamba na kumnunulia gari.
Msanii huyo alisema baada ya kuelezwa na kuukubali ujauzito huo, alimtaka mpenziwe huyo kukaa kimya kwani yeye tayari alikuwa kwenye uhusiano na Zari na hakuwa tayari kuachana na mwanamke huyo aliyemzalia watoto wawili.
Kivumbi kiliibuka upya mwishoni mwa wiki iliyopita, baada ya Hamisa kuvujisha picha alizozipiga kwa siri, akiwa na msanii huyo wa Bongo Fleva, wakiwa kitandani kimahaba, picha ambazo ziliamsha upya gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii, wengi wakimtuhumu msanii huyo kwa kumkana mwanaye wakati ushahidi wote upo wazi.
Ni kelele hizo ndizo zilizomlazimu msanii huyo wa Bongo Fleva kupitia kituo kimoja cha runinga na redio, jana kuibuka na kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu picha zilizovujishwa na Hamisa, ambapo alitumia fursa hiyo kukiri hadharani kwamba yeye ndiye baba wa mtoto huyo.
“Tulikubaliana na Hamisa Mobeto kuwa ujauzito huo usitangazwe kuwa ni wa kwangu, na alikubali,” alinukuliwa msanii huyo. Inadaiwa mwanamitindo huyo hakukubaliana na suala la kufanya mambo yote kuwa siri, hivyo akawa anavujisha taarifa kwa mashosti zake ambao nao walikuwa wakiposti kwenye mitandao ya kijamii, jambo linalotajwa kumtibua msanii huyo na kusababisha apunguze fedha za matumizi mpaka shilingi laki mbili (200,000) kwa mwezi. Hatua ya kupunguziwa matumizi, inatajwa kuwa ilimkasirisha zaidi Hamisa ambaye aliamua kuposti picha zilizowaonesha wakiwa kitandani, ambazo zilichafua hali ya hewa.
Wakati mahojiano hayo yakiendelea redioni, wadau mbalimbali walijitokeza kuzungumzia hali hiyo, lakini wakigawanyika, wengine wakimuunga mkono Hamisa na wengine Zari. Wema Sepetu ambaye uhusiano wake na msanii huyo ulikuwa ndiyo habari ya mjini wakati huo, kupitia akaunti yake ya mtandao wa Instagram, akionekana kumuunga mkono Zari, alisema anatambua wakati mgumu anaoupitia mwanamke huyo aliyempora bwana, katika kipindi hiki kigumu.
“Najua anaweza kusema maneno ya ovyo juu yangu, lakini najua hali anayopitia kama mwanamke, nadhani sasa ni wakati muafaka kwake kuweza kumvisha pete, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni,” aliandika Wema. Huddah Monroe, mwanamitindo kutoka Kenya ambaye naye pia aliwahi kuhusishwa kushiriki mapenzi na msanii huyo, katika namna ya kumpiga kijembe Zari, alisema ‘mwanaume ni wako anapokuwa ndani kwako, akitoka siyo wako’.
Hakuna maoni: