Waziri Mkuu asisitiza kufungua ubalozi wa Tanzania nchini Cuba
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Cuba, Bi. Gladys Bejarano na kumuhakikishia ufunguzi wa ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini humo.
Waziri Mkuu alikutana na Bi. Gladys wakati alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi nchini Cuba. Malengo ya ziara yalikuwa ni kuimarisha na kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
“Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati Tanzania na Cuba, ambayo yalikuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere, hivyo lazima tufungue ofisi za ubalozi na tutamleta balozi wetu hapa.”
Hata hivyo Waziri Mkuu ameishukuru Serikali ya Cuba kwa ujenzi wa kiwanda cha dawa za kuulia vijidudu vya maralia pamoja na ufadhili wa masomo ya udaktari inaoutoa kwa wanafunzi wa Kitanzania ambao wanasoma katika vyuo mbalimbali nchini humo.
Hata hivyo aliiomba Serikali hiyo iendelee kutoa ufadhili wa masomo kwa madaktari hao hadi ngazi ya shahada ya uzamili kwa sababu Serikali ya Tanzania inawahitaji madaktari bingwa wengi kwani walioko nchini ni wachache.
Kwa upande wake, Bi. Gladys alimshukuru Waziri Mkuu kwa kufanya ziara nchini Cuba na alimuhakikishia kwamba uhusiano wa Serikali yake na Serikali ya Tanzania utaendelea kuimarishwa kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Hakuna maoni: